MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wanaingia kambini jioni ya leo katikati ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Fainali hiyo ya Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) itafanyika Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga watamenyana na mahasimu wao wakubwa, Azam FC katika vita ya mataji nchini. 
Yanga itaingia kambini baada ya wachezaji wake kuwasili Dar es Salaam wakitokea Songea ambako walicheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu na kulazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji Majimaji, mabao yao yakifungwa na Paul Nonga na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ kwa penalti.

Wachezaji waliokuwa Songea jana wanaungana na waliobaki Dar es Salaam kuingia kambini leo kwa matayarisho yaa mchezo huo.
Tayari kwa msimu huu Yanga imekwishaizidi kete Azam FC katika mataji mawili, kwanza Ngao ya Jamii Agosti 22, mwaka jana waliposhinda kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0 na baadaye katika Ligi Kuu, ingawa timu hizo zilitoa sare mechi zote mbili, kwanza 1-1 Oktoba 17, mwaka jana na baadaye 2-2 Machi 5, mwaka huu.
Mchezo mwingine uliozikutanisha Yanga na Azam msimu huu ni wa Kombe la Mapinduzi ambao pia zilitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ndani ya dakika 90, hakuna mechi ya Yanga na Azam FC imetoa mbabe msimu huu na mchezo wa keshokutwa kwa kuwa ni wa fainali, unaweza kufika kwenye mikwaju ya penalti pia.
Azam FC na wenyewe baada ya mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu jana wakitoa sare ya 1-1 na Mgambo, wanarudi kambini jioni ya leo makao makuu yao, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza msimu huu, Azam itakutana na Yanga katika bechi la Ufundi kukiwa na mabadiliko, baada ya kundolewa Muingereza Stewart John Hall na timu yake na kuajiriwa Mspanyola Zebensul Hernandez Rodriguez na timu yake.

«
Next

Newer Post

»
Previous

Older Post


No comments:

Leave a Reply