Afrika Kusini na Zimbabwe zimewarejesha nyumbani raia 197 wa Msumbiji. Hayo yamesemwa na Idhaa ya Taifa ya Msumbuji.
Idara ya Taifa ya Uhamiaji nchini Msumbiji imeripoti kuwa, kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, raia 175 wa nchi hiyo walikuwa wameingia nchini kupitia mpaka wa Ressano Garcia wakitokea Afrika Kusini. Taarifa ya idara hiyo imeongeza kuwa, raia 22 wa nchi hiyo wamerejea nchini kufikia mwishoni mwa wiki jana kupitia vituo vya mpakani vya Machipanda na Ponta D'ouro katika mkoa wa Maputo, wakitokea Zimbabwe.
Itakumbukwa kuwa, raia 674 wa Msumbiji walirejeshwa nchini mwao na serikali ya Afrika Kusini mwaka jana 2015. Mamia ya raia wa Msumbuji wanaishi kama wakimbizi katika nchi mbali mbali zinazopakana nayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, mwaka huu pekee, zaidi ya raia 10,000 wa Msumbiji wametorokea nchini Malawi kutokana na machafuko na uhasama kati ya serikali na chama kikuu cha upinzani cha Renamo, haswa katika mkoa wa Tete.
Septemba mwaka jana, Afrika Kusini ilisema kuwa takriban raia 2,600 wa Msumbiji wako katika magereza ya nchi hiyo huku 160 miongoni mwao wakitumikia vifungo vya maisha jela.
Afrika Kusini ni mwenyeji wa raia zaidi ya 40,000 wa Msumbiji, ambapo 32,000 miongoni mwao wanafanya kazi katika migodi na wengine 12,000 ni wakulima.
«
Next

Newer Post

»
Previous

Older Post


No comments:

Leave a Reply