Mrisho  Khalfan  Ngassa

Pamoja na uongozi wa Free State Stars ya Afrika Kusini kumzuia kiungo wake mshambuliaji, Mrisho Ngassa kumtoa kwa mkopo, nyota huyo amewatoa hofu mashabiki wa Yanga na kuwaambia siku si nyingi anarejea kwenye klabu hiyo.

Ngassa ameitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuwasili nchini kisha kutazama mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1.

Ngassa alijiunga na Free State inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, mwaka jana baada ya mkataba wake kumalizika Yanga.

Ngassa amesema viongozi wa Yanga ndio waliowafuata Free State kwa ajili ya kumuomba kwa mkopo ili aiongezee nguvu timu hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ngassa alisema, bado mazungumzo yanaendelea kati ya pande hizo mbili kwa kushirikiana na yeye kuhakikisha anarejea Yanga.

“Nimefurahi sana kuonana na mashabiki wa Yanga na kunifurahia, wengi wao wameonekana kuwa na upendo na mimi waliponiona uwanjani, pia wakinihitaji nirejee kuiongezea nguvu timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa.

“Hivyo niwatoe hofu tu kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri kati ya Yanga na Free State timu inayonimiliki na Mungu akijalia, basi nitarejea kuichezea Yanga,” alisema Ngassa.


Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro alionekana kufichaficha mambo kwa kusema: “Hilo suala bado halijafika mezani kwangu, hivyo siwezi kulizungumzia. Ngassa bado ni mchezaji halali wa Free State, kwa hiyo mambo yakiwa tayari ndiyo naweza kulizungumzia.”
«
Next

Newer Post

»
Previous

Older Post


No comments:

Leave a Reply