Maalim Seif Atikisa Zanzibar, Mabomu Yarindima Kuwatawanya Wafuasi Wake,,,,,,,,
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad jana aliitikisa Zanzibar pale alipoanza ziara yake ya siku sita katika Wilaya ya Kaskazini A na kusababisha polisi kuwatawanya wafuasi wake kwa mabomu na risasi huku baadhi wakijeruhiwa.

Wakati wa ziara hiyo, shughuli za biashara zilisimama kwa muda ili kupisha ziara ya Maalim Seif na mamia ya wananchi wake kwa waume walimpokea na kumfuata kila alipoelekea.

Ulinzi uliimarishwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati wote wa ziara hiyo na vikosi vya ulinzi na usalama vilionekana vikipiga doria kila mahali.

Akiwa Kinyasini, Jimbo la Chaani ambako alifanya kikao cha ndani, wakazi wa eneo la Kivunge kwa mamia walianza kujikusanya katika maeneo ambako Maalim Seif alitarajiwa kutembelea huku wakijipanga barabarani kumsubiri kiongozi huyo. Hata hivyo, askari wenye silaha waliwatawanya.

Katika kuwatawanya, polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi hali iliyosababisha kizaazaa kwa takriban dakika 30 katika eneo la Kivunge kabla ya kurudi hali ya kawaida.

Baada ya hapo baadhi ya askari waliokuwa na silaha waliwazuia waandishi kusogelea eneo hilo wala kuwapiga picha majeruhi.

Mkazi wa Kivunge ambaye alidai ni miongoni mwa watu waliopatwa na mkasa huo, Omari Makame (32) alisema, “Sisi tumejipanga kwa heshima zote kumsubiri kiongozi wetu kipenzi cha Wazanzibari, tukiimba kwa furaha lakini ghafla tumepata kipigo na mabomu ya machozi, nini hiki kama siyo chuki na choyo kibaya.”

Mkazi mwingine, Haji Omar (27) alisema hata baada ya kuwajeruhi wenzao, polisi wali wakatalia kuwapa fomu za kwenda kupata matibabu na hata walipopelekwa hospitali ya Kivunge, polisi walifika na kuwachukua kwa nguvu.

“Wamekataa ushauri wa madaktari wa hapa kwamba wawapeleke Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, lakini wamewachukua kwa nguvu wamekwenda nao Kituo cha Polisi Mkokotoni,” alisema Omar.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi alikiri kuwapo kwa tukio hilo akibainisha kuwa yote hayo yanatokea kwa sababu kuna watu hawataki kufuata sheria, lakini akasema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hassina Tawfik ndiye mwenye nafasi ya kufafanua zaidi.

Juhudi za kumpata Tawfik hazikufanikiwa ikielezwa na baadhi ya watendaji wa ofisi yake kuwa bosi wao hapatikani na hawakuwa na mawasiliano na yeye.

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu wa CUF, Pavu Juma Abdalla alifika katika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushuhudia majeruhi hao wakiwa mikononi mwa polisi.

Waliojeruhiwa ni Makame Abdalla Makame (28), mkazi wa Kivunge Bondeni na Shaame Juma Haji (45) mkazi wa Tumbatu Chwaka.

“Tunapigwa kwa sababu ya umma kuonyesha mapenzi kwa Maalim Seif, wangelikuja watu wa vyama vingine wasingelipigwa lakini ipo siku hawa jamaa wataheshimu haki zetu,” alisema mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Haji akisema baadhi ya majeruhi ni ndugu zake.

Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Salim Bimani ambaye alifika hospitali kuwaona majeruhi alisema:“Wenye mabomu na risasi wamewahujumu watu bure kwa sababu za chuki lakini yote hayo yana mwisho.”.

Bimani alisema Chama chake kinalaani kwa nguvu zote uonevu na hujuma hizo walizo tendewa wananchi wasiokuwa na hatia.

“Tunatumia pia kumbukumbu za hujuma hizi za leo kuongeza ushahidi wa kesi yetu tutakaouwasilisha ICC,” alisema Bimani.

Ziara yenyewe
Maalim Seif alianza ziara hiyo ya kwanza Unguja tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio aliosusa kushiriki katika eneo la Kinyasini, Chaani na kupokewa na mamia ya wafuasi wake ambao walikuwa wakiimba “rais! rais! rais!

Aliambatana na viongozi na watendaji wa CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui; Bimani; Pavu Abdalla na Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi, Omar Ali Shehe.

Aliondoka Kinyansini kuelekea Gamba, Mkwajuni ambako mamia ya wananchi waliokuwa wakimshangilia walijipanga barabarani na walionekana kuongezeka kadri alivyoelekea Kaskazini na kukaribia Jimbo la Mkwajuni.

Baadaye Maalim Seif aliwahutubia wajumbe wa kamati mbalimbali za wilaya na majimbo akieleza kile alichosema ni mwelekeo wa kisiasa wa chama chake, Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Alisema dunia ilishuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki na demokrasia visiwani humo, akidai kwamba pamoja na maonyo ya jamii mbalimbali za kitaifa na kimataifa, watawala waliamua kupora uamuzi wa mamlaka halali ya wananchi kupitia masanduku ya kura ya Oktoba 25, 2015.

“Angalieni watu hawa walivyokosa aibu, umma uliwakataa, mataifa yaliwakataa hata kuwanyima misaada lakini bado hawakuonyesha dalili za kujali kutokana na dhulma waliyotenda.

“Nasema hali hii haitupeleki pema sisi na Taifa kwa ujumla maana iliyoporwa ni haki ya umma na haiwezekani kuisamehe dhambi hii, hivyo mwishowe si mwema na dhuluma haiwezi kudumu kwa muda mrefu asilani, sasa kusema hivyo kuna ubaya gani?”

Hata hivyo, Mwangalizi Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU – EOM) kwa Tanzania, Judith Sargentini amesema atawasilisha ripoti kamili na mapendekezo ya umoja huo, kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana Alhamisi ijayo.

Maalim Seif aliwataka wananchi wote, kama walivyoikataa CCM kabla ya uchaguzi, wakati na baada ya kupiga kura Oktoba mwaka jana, kuunga mkono juhudi na mikakati ya CUF, ili kuhakikisha haki inapatikana, uamuzi wao unaheshimiwa, kwa masilahi ya nchi na Taifa kwa jumla.

Viongozi wa chama hicho Wilaya ya Kaskazini A, walimhakikishia Maalim Seif; “sisi tuko tayari kwa lolote, na naona siyo sisi pekee, kwa sasa kila mtu anaisoma namba, tutakuwa bega kwa bega mpaka haki yetu ipatikane,” alisema Makame Bakari, mmoja wa makatibu wa CUF.
onthespottz.blogspot.com
«
Next

Newer Post

»
Previous

Older Post


No comments:

Leave a Reply